Saturday, 28 December 2019

HOTEL KUBWA ZAIDI DUNIANI kufunguliwa 2020

Abraj Kudai ndio hotel itakayoshikilia rekodi ya ukubwa zaidi duniani pindi itakapoanza kutumika mwaka 2020

Hotel hiyo iliyotengenezwa katika mji wa maka nchi saudia arabia imegharimu Dolar za kimarekan Bilion 3.5 .....itakuwa na vyumba 10,000 na migahawa 70 na maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali

Mji wa Maka una uhakika wa kupokea zaidi ya Mahujaji Milion 2 kila mwaka kwa ajili ya kufanya hija katika mji huo mtukufu wa waislamu

Lakini pia Mji wa Maka kwa mwaka mmoja unapokea zaidi ya Wageni Milion 20 ambao wanakwenda kwa ajili ya kutembea tu

Hotel hiyo itakuwa na vyumba vya kifahari kwa ajili ya watu matajiri, lakini pia kitakuwa na eneo maalumu kwa ajili ya familia ya kifalme ya nchi hiyo

Hotel hiyo imechukua eneo lenye ukubwa wa meter square 1,400,000

Itakuwa majengo marefu 12

Kwa sasa rekodi ya hotel kubwa inashikiliwa na hotel ya Genting Highland ya nchini Malaysia....hotel hiyo ina vyumba 7,351 kwa mchanganuo ufuatao

Standard rooms 3164

Deluxe rooms 2922

Triple deluxe rooms 649

Superior deluxe rooms 480

World club rooms 136

Ukijumlisha vyumba vyote hivi ndio unapata vyumba 7351 vya hotel hii inayoshikilia rekodi ya dunia kwa sasa....hadi hapo Abraj Kudai itakapofunguliwa

Image may contain: sky, cloud and outdoor

WANAUME NDIO WANAUMIA ZAIDI PINDI MAPENZI YANAPOVUNJIKA KULIKO WANAWAKE (ikiwa walikuwa wanapenda)

WANAUME NDIO WANAUMIA ZAIDI PINDI MAPENZI YANAPOVUNJIKA KULIKO WANAWAKE (ikiwa walikuwa wanapenda)
Wanasaikolojia wanasema kuwa pindi mahusiano ya kimapenzi yanapovunjika wanaume ndio wanaumia zaidi kuliko wanawake
Lakini kinachofanya jamii ione wanawake ndio wanaumia zaidi ni kutokana na kuww mwanaume hapendi kuonekana kuwa ameumia kwa ajili ya mapenzi hivyo hujikaza na kujionyeshe usoni kuwa hajaumia
Baada ya mapenz kuvunjika mwanaume huathirika zaidi na ni rahisi kwa mwanaume kujiingiza kwenye tabia zisizofaa pindi anapoumia kwa mapenz kuliko wanawake

VERONIKA SEIDER

.mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuona
Amezaliwa mwaka 1951 nchini ujerumani....na kwa sasa ni Daktar wa meno
Veronika ana uwezo wa kuona mara 20 zaidi ya binadamu wa kawaida
Veronika ana uwezo wa kuwatofautisha watu walio kwenye umbali wa zaidi ya maili moja ......yaan ni sawa na futi 5280
Visual acuity ya binadamu wa kawaida ni 20/20 ......
Lakini yeye ni 20/2

MKUTANO WA SOLVAY WA MWAKA 1927

ulivyowakutanisha watu wenye akili zaidi duniani kwa pamoja
Huu ulikuwa ni muendelezo wa mikutano iliyokuwa inawakutanisha wataalamu waliobobea kwenye taaluma za Fizikia na Kemia wakijadili masuala mbali mbali kuhusu taaluma hizo
Mkutano wa kwanza ulikuwa mwaka 1911 ulifanyika nchini ubelgiji huku mwenyekiti wao akiwa ni Hendrick Lorentz .....katika mkutano huo walijadili kuhusu Quantum Theory na classical physics
Mwaka 1927 ulifanyika mkutano wa tano wa kimataifa wa Solvay ...mkutani huu ukiwakutanisha wanafizikia wa dunia na walioacha historia ya sayansi kuwa hivi ilivyo
Kwenye mkutano huo walikuwa wanajadiliana kuhusu fomula mpya ilioundwa kuhusu nadharia ya quantum ...ambapo Albert Einstein na Niels Bohr ndio walikuwa waongeaji wakuu

Katika mkutano wa mwaka 1927 uliwakutanisha wanasayansi 29 na kati ya hao 17 walishinda tuzo ya noble akiwemo mwanamama Currie aliyeshinda tuzo ya Noble katika taaluma mbili tofauti ya kemia na fizikia
Majina yao kuanzia Nyuma na kuanzia kushoto kwenda kulia
Auguste Piccard, Émile Henriot, Paul Ehrenfest, Édouard Herzen, Théophile de Donder, Erwin Schrödinger, Jules-Émile Verschaffelt, Wolfgang Pauli, Werner Heisenberg, Ralph Howard Fowler, Léon Brillouin,
Peter Debye, Martin Knudsen, William Lawrence Bragg, Hendrik Anthony Kramers, Paul Dirac, Arthur Compton, Louis de Broglie, Max Born, Niels Bohr,
Irving Langmuir, Max Planck, Marie Skłodowska Curie, Hendrik Lorentz, Albert Einstein, Paul Langevin, Charles-Eugène Guye, Charles Thomson Rees Wilson, Owen Willans Richardson

QUEEN ELIZABERTH

Queen Elizabeth ll wa uingereza hapo ni mwaka 1957 baada ya kutoa ujumbe wa Christmass kwenye redio na television

Sunday, 15 December 2019

Je unajua kuwa mchezo wa Kung fu / Wushu umeanzishwa na mtu mwenye asili ya india na sio china kama watu wengi wanavyofahamu

Je unajua kuwa mchezo wa Kung fu / Wushu umeanzishwa na mtu mwenye asili ya india na sio china kama watu wengi wanavyofahamu
Muanzilishi wa Kung fu / wushu anaitwa Bodhidharma ambaye aliishi kati ya karne ya 5 au 6
Inasemekana kuwa alikuwa ni mtoto kutoka katina ufalme wa Pallava wa nchi ya Kanchipuram ....na pia alikuwa muhubiri wa kibudha
Watu wa tibet wanaamini kuwa bodhidharma alikuwa ni mweusi
Wataalamu wametofautiana katika mwaka alioingia china japo wengi wanasema kuwa aliingia china katika utawala wa Liu Song (420-479)...
Na wengine wanasema ni zama za utawala wa Liang ( 502-557)
Haya ndio majina yake mengine anayojulikana kutokana na eneo
1) Japan wanamuita DARUMA
2) Korea wanamuita DALMA
3) Tibet wnamuita DHARMOTTARA
4) Wamalaya wanamuita Dharuma

Kusamehe sio kusahau

Kusamehe sio kusahau
Unapomsamehe mtu haimaanishi kuwa umesahau alichokutendea
Bali maana halisi ya kusamehe ni kuondoa maumivu moyoni mwako...yaan ukiacha kuumia kwa jambo alilokutendea ndio maana halisi ya kusamehe
KWahiyo kusamehe na kusahau ni vitu viwili tofauti

IJUE ARSENAL KWA UCHACHE

1) Ndio timu pekee ambayo haijawahi kushuka daraja tokea msimu wa mwaka 1919/20
2) Katika mechi na shifield united tar 22/1/1927 kwenye uwanja wa highburt ...ndio ikawa mechi ya kwanza ya ligi kuu ya uingereza kutangazwa kwenye redio
3) Arsenal ndio timu pekee kwenye ligi kuu ya uingereza ambayo ilichukuwa ubingwa bila kufungwa ...wakapewa kombe la dhahabu
4)Arsena ndio timu ya kwanza duniani kuonyeshwa kwenye tv ikiwa inacheza mpira ilikuwa ni mwaka 1937
5) 1993 Arsenal ndio timu ya kwanza kuchukua ligi kuu na kombe la Fa ndani ya msimu mmoja
6) Imeitwa Arsenal na jina la utan iwe ni gunners kwa sababu imeundwa na imeundwa na wafanyakazi wa kiwanda cha silaha za kivita woolwich mWaka 1886
7)
8

Thursday, 12 December 2019

Mambo 20 Yakushukuru Kwa Ajili Yake Kwenye Maisha

Asante

Wakati mwingine tunatazama tu mambo ambayo hatuna kwenye maisha, kuliko yale tuliyo nayo. Mara nyingi huwa hatutambui umuhimu wa kitu hadi pale tunapokikosa. Niwazi kuwa wapo watu wanaotafuta vile tunavyoviona ni vidogo lakini hawavipati.
Ni muhimu kutenga muda wa kukumbuka yale mambo yote ambayo tunapaswa kushukuru kwa ajili yake. Kama una chochote kati ya hivi basi yakupasa kushukuru.
  1. Afya njema
    Mara nyingi hatutambui kuwa na afya njema pekee ni jambo muhimu na kubwa sana. Kuna wengi wanaotamani kuwa na afya kama ya kwako lakini hawana; hivyo yakupasa kushukuru kwa afya njema.
  2. Pesa ulizonazo
    Unaweza kufikiri kiasi cha pesa ulizonazo ni kidogo sana hivyo hauhitaji kushukuru. Kuna mahali pengine wewe ni tajiri mkubwa sana. Wapo wasiokuwa na pesa wala chochote kile wanachoweza kukigeuza kuwa pesa.
  3. Marafiki wema
    Marafiki ni muhimu sana kwenye maisha, hasa marafiki wema. Kama una marafiki wanaokutia moyo, kukufariji, kushauri na hata kukusaidia kwa njia moja au nyingine ni jambo la kushukuru.
  4. Wazazi
    Wapo ambao hawakufanikiwa hata kuwafahamu wazazi wao. Lakini kama una nafasi angalau ya kuwa na mzazi hata mmoja ni neema kubwa ambayo yakupasa kushukuru kila wakati.
  5. Kuamka leo
    Je unafahamu kuna wengine walilala lakini hawakuamka? Ni lazima kushukuru kwa kupewa neema ya kuamka tena leo ukiwa mzima. Siyo kwamba wewe unayeishi ni mwema au bora sana bali, ni neema tu.
  6. Makazi na malazi
    Una mahali ambapo unapaita nyumbani? Kama jibu ni Ndiyo, basi una sababu ya kushukuru. Wengine wanahangaika huko na huko bila utulilivu wala mahali ambapo wanaweza kupaita nyumbani. Hawana pa kulala wa pakupumzika.
  7. Mwenzi wa maisha
    Inawezekana uko na mwenzi wako kwenye ndoa lakini unaona ni jambo la kawaida sana; lakini ukumbuke kuwa wapo wengi wanaotamani nafasi hiyo hawaipati. Hivyo ni vyema ukawa na shukurani hata kwa jambo hilo.
  8. Fursa ya kupata elimu
    Sio wote wenye fursa ya kupata elimu. Wengi hukosa fedha au mahitaji muhimu ili kupata hata elimu ya msingi pekee. Hivyo kama umepata elimu kwa kiwango fulani ni jambo la kushukuru pia.
  9. Ulinzi na usalama
    Dunia leo imejaa machafuko ya uhalifu, ugaidi na hata vita. Ikiwa wewe upo kwenye eneo lenye amani na utulivu basi ni jambo la kushukuru.
  10. Maji safi
    Takwimu zinaonyesha kuwa ni watu wachache sana ndiyo wenye fursa ya kupata maji safi duniani. Ikiwa wewe una nafasi ya kupata maji safi kwa ajili ya matumizi yako basi ni jambo la kushukuru
  11. Uwezo wa kuona
    Unaweza kutazama mazingira, watu, wanyama na mambo mengine bila shida? Kama jibu ni ndiyo, basi yakupasa kushukuru kwa hilo pia.
  12. Usafiri binafsi
    Kama una baiskeli, pikipiki au gari basi inakupasa kushukuru kwani wapo wengi wanaopambana usiku na mchana kuvipata lakini bado hawajafanikiwa.
  13. Uhuru wa kujieleza
    Kuna nchi na maeneo ambayo uhuru wa watu wa kujieleza umebanwa sana. Hivyo ukiwa na uhuru wa kuongea na kujieleza basi yakupasa kushukuru kwa hilo.
  14. Uhuru wa kuabudu
    Je unaweza kuabudu mahali upatakapo au kwa namna unayopenda bila shida? Hili ni jambo ambalo watu wengi wanalikosa. Wengi hulazimishwa kuabudu sehemu fulani au huzuiwa kuabudu kabisa. Ikiwa una uhuru wa kuabudu basi yakupasa kushukuru.
  15. Uwezo wa kusikia
    Wapo watu wanaotamani kusikia nyimbo nzuri au sauti nzuri za ndege na wanyama lakini hawawezi. Hivyo ni vyema ukashukuru ikiwa wewe una uwezo wa kusikia vyema.
  16. Watoto
    Watoto ni baraka na zawadi kubwa. Wengi huwaona kama watu wasiofa lakini kwa wengine ni lulu. Mara nyingi watu hawatambui thamani ya watoto hadi pale wanapowakosa. Ni muhimu kushukuru kwa zawadi hii kubwa.Mawasiliano
  17. Una simu, kompyuta, tablate n.k vinavyokuwezesha kuwasiliana au eneo ulilopo lina mawasiliao mazuri? Kama una vitu hivi ni muhimu kushukuru kwani dunia ama ulimwengu usiokuwa na mawasiliano ni mgumu sana.
  18. Changamoto
    Changamoto? Ndiyo, changamoto ni jambo la kushukuru kwa ajili yake kwa kuwa zinakupa hamasa ya kuendelea mbele ili uwe bora zaidi. Kusingekuwa na changamoto watu wasingefanya jitihada zozote kuboresha maisha yao.
  19. Mavazi
    Umeshafikiri kuwa fasheni au mitindo katika mavazi siyo lazima? Jambo la msingi ni kufunika mwili wako dhidi ya jua, mvua, wadudu pamoja na kutunza staha yako tu. Ikiwa una mavazi kwa ajili ya kujisitiri ni jambo kubwa sana linalo kupasa kushukuru.
  20. Uhuru wa kupiga kura
    Kutokana na kiu na uchu wa madaraka, mifumo halali ya kupata viongozi imeingiliwa sana. Siyo kila mtu duniani ana uhuru wa kupiga kura kwa amani ili kumchagua kiongozi anayemtaka. Ikiwa wewe una nafasi hiyo, hata kama hauitumii ni jambo la kushukuru pia.
Neno la Mwisho
Naamini yapo mengi zaidi na zaidi yakushukuriwa. Ni vyema tukajifunza kushukuru ili tufungue milango ya kupata mengine mazuri zaidi. Kuacha kulalamika na kuona angalau yale mazuri mchache ni jambo la msingi.
Je wewe huwa unashukuru kwa haya? Je kuna jambo gani jingine muhimu la kushukuru? Tafadhali tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine makala hii.

Mpiga Ngoma Maarufu wa Mtaani Anayetengeneza Midundo kwa Kutumia Ndoo

Gordo


Nani anahitaji ngoma wakati anaweza kutumia ndoo kutengeneza sauti na midundo ya pekee? Mpiga ngoma wa mtaani kule Australia aitwaye Gordo, ambaye awali alisoma nchini Japan, anafahamu kuwa inawezekana kutengeneza muziki kutoka kwenye kila kitu bila tatizo lolote.
Akiwa mwenye nguvu, nia na shauku, Gordo anaonekana akitumia ndoo, vijiti vya kupigia ngoma na miguu yake kutengeneza midundo mizuri ya ngoma.
Ikiwa hana shughuli na wasanii wengine, mwaliko kwenye tukio au sherehe basi utamkuta Gordo akiwa kwenye mitaa ya Sydney akidhihirisha kipaji chake katika jamii.
Watu wengi huvutiwa na kipaji chake na hata kumzawadia pesa na vitu vingine; naamini hata wewe utakapotazama video zake hapa chini, hakika atakuvutia na kukuhamasisha sana

Tuesday, 10 December 2019

Mambo 18 ya Kushangaza Kuhusu Intaneti Usiyoyajua

Intaneti

Hivi leo kuna mambo mengi kuhusu intaneti, lakini hapa nitakuonyesha baadhi ya mambo ambayo naamini yatakuvutia na kukushangaza. Historia ya intaneti inaanzia miaka ya 1950 ikienda sambamba na maendeleo ya kompyuta.
Ni wazi kuwa, ulimwengu wa intaneti wa leo ulianzwa na mwanasayansi wa kompyuta wa Uingereza Tim Berners-Lee. Kuundwa kwa intaneti yake ya kwanza, moja kwa moja kulibadili ulimwengu, vyombo vya habari, mahusiano, burudani na mambo mengine mengi.
Tunapotazama intaneti leo, ni wazi kuwa tunaona mambo mengi ambayo intaneti imepitia tokea kuanzishwa kwake hadi hivi leo. Karibu ufuatilie makala hii ili ufahamu mambo 18 ya kushangaza kuhusu intaneti usiyoyajua.

1. Tovuti ya kwanza bado ipo

Tovuti ya kwanza kutengenezwa bado ipo na inafanya kazi hadi leo. Jambo pekee ni kuwa tovuti hiyo inaonekana vile vile kama ilivyokuwa zamani. Unaweza kutembelea hapa ili kuiona.Tovuti ya kwanza

2. Takriban barua pepe bilioni 247 hutumwa kwa siku

Kampuni ya Radicati inakadiria kuwa takriban barua pepe bilioni 247 hutumwa kila siku. Inaelezwa kuwa asilimia 90 ya barua pepe hizo ni barua pepe hatarishi (SPAM) na Virusi, hivyo kuwa makini na barua pepe unazofungua.Barua pepe

3. Tweet ya kwanza ilichapishwa Machi 21, 2006 na Jack Dorsey

Nani alifahamu kuwa Twitter ingekuwa maarufu duniani kama ilivyo leo? Mnamo Machi 21, 2006 Jack Dorsey aliandika tweet ya kwanza iliyokuwa inasema, “Just setting up my twttr.” lakini hivi leo Twitter imeshakuwa na mamilioni ya watumiaji ulimwenguni kote.Twitter

4. Video iliyotazamwa kuliko zote kwenye mtandao ni Despacito

Wimbo wa Despacito ulioimbwa na Luis Fonsi na Daddy Yankee ni wimbo unaoongoza kwa kutazamwa na watu wengi zaidi kwenye mtandao wa YouTube. Wimbo huu umeshatazamwa mara bilioni 3.55 hadi sasa.

5. Mgunduzi wa intaneti Tim Berners-Lee alipewa cheo cha Knight na malikia Elizabeth

Kutokana na ugunduzi mkubwa alioufanya Tim Berners-Lee, malikia Elizabeth wa Uingereza alimpa cheo cha Knight kwenye serikali yake mwaka 2003.Mwanzilishi wa Intaneti

6. Saa 300 za video hupakiwa kila dakika kwenye YouTube

YouTube ni mtandao maarufu ambao wengi wanaufahamu kama mtandao wa kusambaza na kutazama video kwenye mtandao. Lakini je unajua kuwa kwa muda wa dakika moja video zenye jumla ya urefu wa saa 300 hupakiwa katika mtandao huu? Tovuti hii hupokea video kutoka kwa watumiaji mbalimbali duniani kote.YouTube

7. Neno kuperuzi mtandao (Surfing the internet) liliundwa mwaka 1992

Kabla ya mwaka 1992 neno (surfing the internet) halikuwa linafahamika hadi pale Jean Polly alipoandika makala iliyosomwa sana na kupakuliwa na watu wengi na kusababisha kusambaa kwa neno hili.

8. Mitandao ya kutafuta wapenzi inazalisha takriban dola bilioni 2.2 kila mwaka

Teknolojia imebadili mfumo wa maisha. Watu hutafuta wapenzi au wenzi wa maisha kwenye mtandao. Hili limepelekea tovuti za kutafuta wapenzi kuzalisha zaidi ya bilioni 2.2 kwa mwaka 2014 pekee.

9. Asilimia 10 ya wahalifu wa kijinsia wanatumia mitandao ya kutafuta wapenzi

Kutokana na umbali au kutokufahamiana vyema, wahalifu wengi wa kijinsia hutumia mitandao ya kutafuta wapenzi kufanya uhalifu wao.

10. Takriban Watoto milioni moja wamezaliwa kutokana na watu waliokutana kupitia Match.com

Mtandao wa match.com unadai kuwa takriban watoto milioni moja wamezaliwa kutokana na watu waliokutana kwenye tovuti hiyo ya kutafuta wapenzi.Mtoto

11. China ina kambi za kutibu waathirika wa kutawaliwa na mtandao (internet addict)

Wakati china ikiwa na watumiaji wa intaneti wapatao zaidi ya milioni 721, inaaminika kati yao milioni 23 ni waathirika wa kutawaliwa na mtandao. Hivyo wameanzisha kambi mbalimbali za kuwasaidia watu hawa.

12. Watumiaji wengi wa intaneti ni roboti na programu haribifu (malware)

Wakati mwingine unaweza kufikiri watumiaji wa mtandao ni watu pekee. Lakini asilimia kubwa ni roboti na programu haribifu zilizobuniwa na watu mbalimbali ili kutimiza shughuli fulani.Roboti

13. Tweets milioni 500 zinatumwa kila siku

Kutokana na Twitter kuwa na watumiaji milioni kadhaa, inaaminika kuwa zaidi ya tweets milioni 500 hutumwa kila siku.

14. Huwa unatumia kisehemu kidogo tu cha mtandao

Ni wazi kuwa sehemu unayoitumia kwenye intaneti ni sehemu ndogo sana ambayo inaonekana kwenye injili pekuzi (search engines). Ipo sehemu nyingine ambayo imefichwa kwenye injini pekuzi (dark web); sehemu hii inajumuisha taarifa binafsi za watu, taasisi na makampuni mbalimbali. Unaweza kuperuzi sehemu iliyofichwa ya intaneti kwa kutumia kivinjari (browser) ya Tor.

15. Tovuti 30,000 zinadukuliwa kila siku

Kutokana na kuongezeka kwa uhalifu wa kwenye mtandao, inakadiriwa kuwa zaidi ya tovuti 30,000 hudukuliwa na wadukuzi kila siku.

16. IMDb ilikuwepo tangu miaka ya 1990

Tovuti maarufu ya kutafuta video, filamu, vipindi vya televisheni pamoja na michezo ya video ilianzishwa mnamo Oktoba 21, 1990, na Col Needham. Baada ya miaka minne ilipata jina lake la IMDb ambalo imedumu nalo hadi leo.

17. Tovuti milioni 7 zilifungwa mwaka 2009

Huduma ya GeoCities ya Yahoo iliyokuwa inawaruhusu watu kutengeneza tovuti zao binafsi ilifungwa mwaka 2009 na kupelekea kufutwa kwa zaidi ya tovuti milioni 7. Tovuti hizi zilifutwa kutokana na kuwepo kwa tovuti nyingi zilizokuwa na ubora duni.

18. Watu takriban asilimia 100 wa Iceland  wanatumia intaneti

Nchi nzima ipo kwenye mtandao? Ndiyo, nchi ya Iceland ina wakazi wapatao 331,778 ambao takriban wote wanatumia mtandao wa intaneti. Je nchi yako ni ya ngapi? Unaweza kutazama hapa.Iceland
Hitimisho
Naamini umejifunza mambo kadhaa mapya kuhusu mtandao wa intaneti. Ni wazi kuwa safari ya maendeleo yaliyofanyika kwenye mtandao wa intaneti ni ndefu na ina mabo mengi sana ya kusisimua.

Saturday, 7 December 2019

Mambo 17 ya Kuzingatia Kabla ya Kusafiri Kwenda Nchi Nyingine

Ndege

Safari ni jambo linalohitaji maandalizi, hasa safari ya kwenda nchi nyingine. Watu wengi hujikuta wakiingia kwenye matatizo mbalimbali kutokana na kutokufahamu mambo ya kuzingatia kabla ya safari.
Ikiwa umeshasafiri, au ni mara yako ya kwanza kusafiri kwenda nchi nyingine, basi karibu nikushirikishe mambo 17 ya kuzingatia kabla ya kusafiri kwenda nchi nyingine.

1. Hakiki muda wa mwisho wa pasi yako ya kusafiria

Kama una pasi ya kusafiria, hakikisha muda wake wa matumizi haujakaribia kwisha. Hakikisha pia kurasa zilizo wazi hazijakaribia kwisha.
Kumbuka kuwa baadhi ya nchi haziruhusu watu kuingia au kutoka kwa kutumia pasi za kusafiria zilizobakiza muda wa miezi 6 kuisha muda wake.

2. Fahamu nyaraka zinazohitajika

Kila nchi ina taratibu na sheria zake. Hivyo hakikisha nyaraka kama vile VISA unazifuatilia kabla ya kwenda kwenye nchi inayohitaji nyaraka hizo.

3. Fahamu hali ya kisiasa na kiafya ya nchi husika

Hali ya kisiasa na kiafya inatofautiana kati ya nchi moja hadi nyingine. Kusafiri kwenda kwenye nchi yenye machafuko ya kisiasa au magonjwa hatari kama vile Ebola, unatakiwa kuchukua tahadharikubwa zaidi.
Hakikisha unaweza kustahimili na umejiandaa vyema kukabiliana na hali ya kisiasa na kiafya ya nchi unayokwenda kabla ya kuanza safari.

4. Fanya uchunguzi wa kiafya

Ni muhimu kumwona daktari kabla ya kusafiri ili achunguze kama kuna tatizo linaloweza kukukabili utakapokuwa nchi ya kigeni.
Pia chunguza kama utaweza kupata huduma za kimatibabu pindi uwapo katika nchi husika unayokwenda.

5. Kuwa na nakala za nyaraka muhimu

Lolote linaweza kutokea pindi uwapo safarini, nyaraka zako muhimu zinaweza kuibiwa au kupotea; hivyo ni muhimu kuwa na nakala za nyaraka zako muhimu.

6. Kuwa na fedha za dharura mkononi

Usitegemee sana mifumo ya kielektroniki kupata pesa pindi uwapo nje ya nchi.
Hakikisha unabeba kiasi fulani cha pesa mkononi mwako ili uweze kukidhi mahitaji yako pale utakapokosa pesa kwa kupitia njia za kawaida.
Chunguza kama utaweza kubadilisha pesa zako katika nchi unayokwenda ili kupata pesa za nchi husika. Ikiwa haiwezekani kubadilisha pesa zako katika nchi husika, basi badili pesa zako kabla ya safari.

7. Chunguza mambo au vitu vinavyoruhusiwa katika nchi husika

Vitu, mambo au tabia fulani ambazo ni halali au za kawaida kwenye nchi yako zinaweza zikawa mbaya au zisizo halali kwenye nchi nyingine.
Kwa mfano kuna nchi ambazo ni marufuku kumkumbatia mwanamke au mwanamke kuendesha gari. Pia kuna nchi ambazo huwezi kubeba vitu kama mbegu fulani, mawe au hata dawa fulani. Hivyo chunguza hili kwanza.

8. Tafiti kuhusu hoteli na vyakula

Ikiwa umepanga kwenda kukaa hotelini, ni muhimu kuhakikisha unafahamu utakavyofika hotelini na gharama husika za kukaa hapo.
Ni muhimu pia kufahamu kuhusu vyakula, kwani baadhi ya vyakula vya kigeni vinaweza visikufae; hivyo chunguza utakachokula na utakavyokipata.

9. Fahamu kanuni za usafiri utakaoutumia

Kwa mfano kama utatumia usafiri wa ndege ni muhimu ukafahamu sheria za ndege husika. Mara nyingi ndege haziruhusu kubeba madawa, silaha, mizigo mikubwa au hata baadhi ya vifaa vya kielektroniki.
Ili kuepuka kukwama kwenye safari yako. Ni muhimu ukafahamu swala hili mapema.

10. Fahamu utakavyopata huduma zako za kifedha

Kama unatumia kadi za kibenki kupata pesa, ni muhimu ukahakikisha kama utaweza kuzitumia kwenye nchi unayokwenda. Kwa mfano nchini Iran hakuna huduma za fedha za kimataifa.
Hivyo ni muhimu kuchukua hatua mapema kuhakikisha huduma au njia unayoitumia kupata pesa inapatikana kwenye nchi husika.

11. Beba vifaa vya mbadala vya kielektroniki

Viwango vya umeme (voltage) pamoja na viunganishi vyake (plugs) hutofautiana baina ya nchi moja na nyingine. Kwa mfano nchini Marekani, viwango vya umeme pamoja na viunganishi vyake ni tofauti sana na vile vya nchi za Afrika Mashariki.
Hivyo ili kuhakikisha unaweza kutumia vifaa vyako vya kielektroniki, ni vyema ukabeba vifaa vitakavyokuwezesha kuendana na mazingira husika. Mf. World travel adapter au multipurpose adapter

12. Fahamu kuhusu huduma za mawasiliano

Ni wazi kuwa uwapo katika nchi nyingine utahitaji huduma za mawasiliano kama vile intaneti na simu. Ni muhimu ukafahamu njia utakazotumia kupata huduma hizi pamoja na gharama zake.
Hakikisha kama eneo utakalokuwa lina mawasiliano, na kama halina mawasiliano fahamu njia mbadala utakayoitumia kuwasiliana.

13. Tafuta washauri wa safari

Zipo kampuni kadha wa kadha kwenye kila nchi zinazojihusisha na utalii au kuongoza safari. Unaweza kutafuta kampuni moja ikakupa muongozo au taarifa za muhimu kuhusu safari pamoja na nchi unayokwenda.
Ikiwa pia una mtu unayemfahamu katika nchi unayokwenda, unaweza kumtumia kupata taarifa.

14. Tafiti kuhusu hali ya hewa

Hebu fikiri unaenda kwenye nchi ya baridi kali bila nguo za kujikinga na baridi; je huoni kuwa utapata shida?
Hakikisha unafahamu vyema hali ya hewa ya eneo unalokwenda kama ni ya joto, baridi, mvua, upepo, barafu  n.k. Kwa njia hii utaweza kujiandaa na kuchukua tahadhari stahiki mapema.

15. Jifunze misamiati michache ya kigeni

Inawezekana unakwenda kwenye nchi inayotumia lugha tofauti na ya kwako; hakikisha unajifunza misamiati michache ya lugha ya nchi hiyo hatakama utakuwa na mkalimani.
Kujifunza misamiati michache ya lugha ya nchi husika kutakusaidia kujiandaa kwa lolote litakalotokea, ukipata shida uweze kujieleza au hata kuoyesha ukaribu kwa wenyeji wako.

16. Beba dawa muhimu

Nibebe dawa tena? Ndiyo, kwani uzima uko mikononi mwako? Kumbuka ni muhimu kubeba dawa za muhimu kama vile dawa za kutuliza maumivu.
Unapokuwa katika nchi nyingine unaweza kupatwa na maumivu na ukakosa dawa kwa karibu; hivyo kubeba dawa kutakusaidia sana.

17. Tafuta vitabu vya miongozo ya safari

Vipo vitabu mbalimbali vinavyotoa miongozo ya safari katika nchi mbalimbali duniani. Vitabu hivi hupatikana pia kwenye mtandao au maghala ya programu za simu za kisasa (App Store na Play store).
Kwa kuwa na vitabu hivi, utaweza kupata taarifa na miongozo mbalimbali kabla na uwapo safarini.
Hitimisho
Naamini sasa umefahamu au kukumbushwa juu ya mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kusafiri kwenda nchi nyingine. Naamini ukizingatia mambo haya kwa makini, utaweza kuwa na safari njema yenye amani na furaha.
Ninajua unajiandaa na safari au utajiandaa hivi karibuni; hivyo ninakutakia safari njema yenye amani na furaha.

Faida 10 za Kusafiri Unazotakiwa Kuzifahamu

tembo

Najua umeshajiuliza faida za kusafiri? Ndiyo, kusafiri kuna faida nyingi unazopaswa kuzifahamu. Swala la kusafiri au kutembelea maeneo mbalimbali halijazoeleka sana kwetu waafrika kama ilivyo kwa wenzetu wazungu.
Kusafiri siyo lazima kwenda nchi nyingine, bali hata safari za ndani ya nchi au za ndani ya eneo lako zina maana kubwa. Kwa hakika zipo sababu kuntu zinazowafanya wenzetu wa magharibi kusafiri kwenda sehemu mbalimbali duniani. Ikiwa basi unataka kufahamu faida za kusafiri ili uzifanyie kazi, basi karibu nikushirikishe faida 10 za kusafiri.

1. Kujifunza mambo mbalimbali

Unaposafiri unajifunza mambo mbalimbali ambayo isingekuwa rahisi kujifunza mambo hayo ukiwa nyumbani.
Unaposafiri utajifunza jografia, utamaduni au hata mtindo wa maisha wa watu wa eneo utakalotembelea. Hivyo basi, kusafiri ni shule nzuri ya kuongeza maarifa yako.

2. Kupata marafiki

Kwa njia ya kusafiri utapata marafiki mbalimbali ambao watatokana na watu uliokutana nao safarini. Zipo shuhuda kadhaa za watu waliopata marafiki kwenye safari zao waliowafaa katika maisha yao yote.
Pia wapo watu waliopata wenzi wa maisha kutokana na kusafiri; hivyo faida hii ya kusafiri haiwezi kuachwa nyuma.

3. Kufahamu fursa mpya

Huwezi kufahamu vyema fursa zilizoko kwenye eneo fulani kama hutokwenda kwenye eneo hilo. Kwa njia ya kusafiri utaweza kuona fursa mbalimbali ambazo unaweza kuzifanyia kazi na ukajipatia kipato au ukaongeza kipato chako.
Hapa naikumbuka kampuni ya kitalii ya Bob Africa ambayo ilianzishwa na wanandoa wawili waliokuja Afrika kama watalii na baadaye wakaona fursa ya kuwekeza kwenye utalii.

4. Kujifunza lugha mpya

Unaposafiri kwenda nchi nyingine inayozungumza lugha tofauti na ya kwako ni lazima ujifunze lugha ya nchi husika angalau kwa uchache.
Hivyo, kwa njia hii utaongeza idadi ya lugha unazozifahamu na kuwa mwenye tija zaidi.

5. Hukupa mtazamo mpya

Faida nyingine ya kusafiri ni kupata mtazamo mpya tofauti na ule uliokuwa nao awali. Inawezekana kuna mambo ambayo huwa huyathamini uwapo nyumbani, lakini utayathamini uwapo safarini.
Inawezekana pia ulikuwa na mtazamo fulani kuhusu watu au eneo fulani, lakini utapata mtazamo mpya baada ya kusafiri kwenda eneo husika.

6. Hukuwezesha kutumia muda vyema

Inawezekana umepata likizo fupi au una muda fulani wa mapumziko kila baada ya kipindi fulani; badala ya kutumia muda wako kulala au kutazama televisheni siku nzima, unaweza kuutumia muda huo kwa kusafiri.
Hivyo, hutopoteza tena muda wako kwenye mambo yasiyo na tija, bali utautumia muda wako kwa mambo yenye manufaa kwako.

7. Huondoa msongo wa mawazo

Msongo wa mawazo ni tatizo kubwa linalowatesa watu wengi kwenye dunia hii ya leo. Kwa njia ya kusafiri utaweza kuondoka kwenye mazingira au katikati ya watu wanaokufanya upate msongo wa mawazo.
Hivyo, unaposafiri utaona mambo au mazingira tofauti ambayo yatabadili hali yako ya kisaikolojia na kukuepushia msongo wa mawazo.

8. Hukuwekea kumbukumbu ya kipekee

Hebu fikiri ukisafiri na kwenda kukwea mlima Kilimanjaro au Evarest, naamini hili litakutengenezea kumbukumbu ambayo siyo rahisi kusahaulika.
Mambo uliyoyafanya na kuyaona au hata jinsi ulivyokabiliana na changamoto mbalimbali kutakutengenezea kumbukumbu nzuri ya kipekee.

9. Hukuburudisha.

Kusafiri ni burudani ya aina yake hasa kama unasafiri kwenda kwenye eneo sahihi. Unaposafiri utapata faida ya kupata burudani bora na ya kipekee.
Uwapo safarini utaweza kuona vitu vya kuvutia kama vile mazingira ya asili (mito, milima, mabonde, n.k.), wanyama pamoja na sanaa za eneo husika kama vile ngoma, maigizo, mavazi ya kitamaduni, n.k.

10. Huboresha maisha ya wengine

Unaposafiri unaweza kuboresha maisha ya watu wengine kwa njia moja au nyingine.
Hebu fikiri juu ya vyombo vya usafiri unavyovitumia, hoteli, viingilio utakavyolipa, n.k. Hivi vyote vinawapa kipato watu wengine na kuboresha maisha yao.
Hivyo, kusafiri hakukunufaishi wewe peke yako bali hata na wengine wanaohusika kwenye safari yako.
Hitimisho
Kwa hakika unaweza kutazama swala la kusafiri kwa juu juu na kufikiri halina faida yoyote. Ni ukweli usiopingika kuwa wenzetu wazungu wanafahamu vyema umuhimu wa kusafiri ndiyo mana wako tayari kulipa gharama kubwa ili watimize lengo lao.